Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjuma cha Shirika la Habari la Hawza, Sheikh Ali Al-Khatib, Naibu Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Mashia, katika hotuba yake aliyotoa kwenye hafla ya uzinduzi wa ensaiklopidia ya «Ufafanuzi wa Kitabu cha Nahjul-Balagha», iliyofanyika Jumatano usiku, tarehe 25 Novemba 2026 (4 Azar 1405 Hijria Shamsia), iliyoandaliwa na Hizbullah, alisema: “Leo hii tunashuhudia sherehe na mafanikio makubwa ya kielimu yaliyofikiwa na Shahidi Sayyid Hashim Safiuddin. Yeye alikusudia kukifanya kitabu cha Nahjul-Balagha kuwa mradi wa kimawazo na kielimu, ambao kazi ya kuuandaa ilichukua miaka mingi.”
Alibainisha kuwa; kujishughulisha kwa Shahidi Sayyid Safiuddin na kazi ya kufafanua kitabu cha Nahjul-Balagha hakukuwa tu ni kazi ya kuhifadhi kumbukumbu na kukusanya taarifa, bali ulikuwa ni mradi wa kielimu na kimalezi ndani ya shule ya Imam Amirul-Muuminina (as).
Sheikh Al-Khatib, akiwahutubia wanazuoni na ndugu walioibeba amana hiyo na kuendeleza njia aliyoiweka ili kukamilisha kazi hii, na hivyo kuifanya kuwa matunda ya juhudi za pamoja na uaminifu kwa shahidi huyo, alisema kuwa; Shahidi Sayyid Safiuddin hakutosheka tu na kuitumikia dini na kufanya jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu, pamoja na kuwahudumia wanadamu, bali aliingia pia katika uwanja wa kielimu ambao wanazuoni wakubwa hushindana ndani yake. Ni uwanja ambao elimu huunganishwa na matendo, na utafiti wa kielimu huunganishwa na jihadi.
Aliongeza kuwa: “Kupitia shakhsia ya Shahidi Sayyid, tunakumbuka kwamba elimu haipaswi kubaki imefungiwa ndani ya mipaka ya darsa na masomo pekee, bali inapaswa kugeuzwa kuwa matendo. Na hapa ndipo yale aliyoyafanya mwanazuoni huyo shahidi yanapokutana na mafundisho ya shule ya Imam Amirul-Muuminina Ali (as).”
Naibu Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Mashia alisisitiza pia kwamba mataifa hayajengwi kwa nguvu na utawala wa kimabavu pekee, bali hujengwa kupitia elimu, maadili na utashi wa kweli unaomfanya mwanadamu kuwa nguzo kuu katika kila mradi wa kitaifa.
Alieleza kuwa watu huondoka duniani, lakini yale wanayoyaacha nyuma katika elimu na fikra hubaki milele, yakiwa ni sadaka yenye kuendelea kupata thawabu, ambayo athari zake hazikatiki.
Sheikh Al-Khatib alihitimisha hotuba yake kwa kusema: “Ewe Sayyid Hashim! Ninakupongeza kwa kuwa uliweza kuunganisha huduma na jihadi, na ukarejea kwa Mwenyezi Mungu katika hali ya kuwa shahidi; ukiwa ni mwanazuoni mwenye kutekeleza kwa vitendo yale aliyoyajua, ambae alikuwa katika kuutumikia Umma, taifa lake na ujumbe wake wa kidini.
Ulikuwa ukibeba changamoto na matatizo ya wananchi kama amana mikononi mwako, sambamba na rafiki yako wa safari hii, Mtukufu Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Hassan Nasrullah.”
Maoni yako